Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea taarifa juu ya
mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Young Africans SC kushawishi
mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni
ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika
ngazi ya makundi kati ya Young Africans ya Tanzania na TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) utakaofanyika Juni 28, 2016 saa
10.00 jioni kwenye Uwanja wa Dar es Salaam.
TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara
moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young
Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni
kinyume na kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua
hii.
Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na
masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha
matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya
televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au
wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa
faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni.
Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani
ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya
hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Young Africans
walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala
ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora.Wapenzi wa Yanga
wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu timu yao ikiwa ni
njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata
sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi.
Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika
taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo,
Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji,
Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo
KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO. Vilevile vitendo vya kutishia
amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa
taratibu za kijinai.
Katika mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na
Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa
kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto
(line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba.
Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016.
Taarifa zaidi itatolewa karibuni.
Post a Comment