Kiwango kizuri cha kulala kinachopendekezwa kwa kila mmoja ni saa 7 hadi 8 kila usiku unapoingia, kwa mujibu wa mwandishi wa ripoti ya utafiti huo, Lauren Wise, ambaye ni profesa katika Shule ya Afya ya Umma katika Chuo Kikuu cha Boston, Marekani.
Kwa mujibu wa Wise, kati ya jozi 790 za wapendanao, watafiti wamebaini kuwa kulala kwa muda mfupi au kulala kwa muda mrefu – yaani chini ya masaa 6 au masaa 9na zaidi kwa usiku mmoja -- kulikuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja na kupungua kwa uwezo wa kupata ujauzito."
Kwa kuzingatia ulalaji wa masaa nane kama rejea, wanaume ambao hulala kwa masaa chini ya sita au wanaolala kwa zaidi ya masaa tisa kila usiku unapoingia "walikuwa na asilimia 42 ya kupungukiwa na uwezo wa kuwapa ujauzito wenzi wao katika mwezi wowote ule wa kujamiiana," aliongeza.
Sababu kubwa inayotolewa ni kwamba kulala bila kuzingatia muda maalumu huathiri vichocheo vya mwili, kwa mujibu wa Wise. Wataalamu wa masuala ya uzazi wanajua kwamba vichocheo vya wmili viitwavyo ‘testosterone’ ni muhimu kwa uzalishaji wa mbegu na sehemu kubwa ya mbegu hizo huzalishwa kwa wanaume wakati wa kulala, alisema.
Jumla ya muda wa kulala kwa wanaume umekuwa na uhusianao chanya na kiwango cha testosterone kupitia ripoti za tafiti mbalimbali, aliongeza. Wapendano wote katika utafiti walikuwa wakijaribu kupata mimba, na wamekuwa wakijaribu kufanikisha lengo hilo kwa zaidi ya mizunguko sita ya mwezi ya kina mama.
Wahusika walijibu maswali kuhusiana na ratiba zao za kulala na ikiwa walipata usingizi kwa taabu. Wanaume wote waliokuwa na wakati mgumu katika kulala walikutwa pia wakiwa na uwewekano mkubwa zaidi wa kushindwa kuwapa ujauzito wenzi wao kulinganisha na wale waliolala wa raha mustarehe, utafiti ulibaini.
Wakati utafiti ulibaini uhusiano tu wa kulala na ujauzito, "haukuweza kuthibitisha chanzo na athari zake," alisema Wise.
Lakini uhusiano huo uliendelea hata baada ya kuzingatia pia umri wa wanaume na wanawake, uzito wao kulinganisha na urefu wa mwili, idadi waliyokuwa wakikutana, na sababu nyingine zinazojulikana kuwa huathiri afya ya uzazi.
Tafiti zaidi zinahitajika, Wise alisema. "Inawezekana kwamba kukosa usingizi wa kutosha kunaweza kusababisha mwenendo mbaya kiafya wa maisha, kupungua kwa nishati mwilini na kupungua kwa nguvu ya tendo la ndoa…lakini tulijitahidi kudhibiti hizo sababu nyingine zote," alisema.
Matokeo hayo ni habari njema kwa Dk. Peter Schlegel, Makamu wa Rais wa taasisi ya Tiba ya Afya ya Uzazi Marekani.
"Kuna takwimu chache sana kuhusiana na namna usingizi unavyoweza kuathiri uwezo wa kuzaa wa wanaume," alisema.
"Tunajua kwamba msongo wowote wa mawazo huweza kuathiri afya ya uzazi ya wote, yaani wanawake na wanaume. Utafiti huu unaonyesha kwa kiwango kikubwa kwamba wanaume, wanaolala kati ya masaa saba hadi chini ya masaa tisa huwa wanaimarisha afya yao ya uzazi na hivyo kujiongezea uwezekano wa kuwapa mimba wapenzi wao pindi wanapokubaliana kufanya hivyo.”
Kwa kuangalia matokeo ya utafiti huo mpya, madaktari wanaowashauri wapendanao wanapaswa sasa kuzungumzia kuhusu kiwango cha usingizi ambao wanaume wanapaswa kuwa nacho,” alisema Schlegel.
Na kwa wanawake, "hatujui kwakweli," alisema. Tafiti nyingine zinaonyesha kwamba kula matunda na mbogamboga zaidi kuboresha uzalishaji wa mbegu za kina baba kuliko nyama na mafuta, alisema Schlegel, ambaye ni mwenyekiti katika taasisi ya tiba ya Weill Cornell jijini New York City.
Tatizo pekee katika utafiti huo, Schlegel alisema, ni kwamba watafiti hawakupima idadi ya mbegu.
Utafiti huo ulikuwa uwasilishwe Jumatano kwenye mkutano wa mwaka wa taasisi ya tiba ya afya ya Marekani, mjini Salt Lake. Utafiti unaowasilishwa kwenye mkutano wa tiba huchukuliwa kuwa ni wa awali hadi unapochapishwa katika jarida la masuala ya tiba linalopitiwa na wataalamu mbalimbali afya. Asaaante kwa kutembelea Lang Media Tz kwa Habari nyingine Nyingi ungana nasi kupitia Account zetu Facebook, Twitter, na Instagram
Post a Comment