*Apigilia msumari wanafunzi UDOM kutimuliwa
NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amesema Rais mstaafu Jakaya Kikwete amemwachia kazi ngumu, ikiwamo ya kulipia ada wanafunzi ‘vilaza’ waliofukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Alisema hayo jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya chuo hicho.
“Wanasiasa wana maneno, wanataka waliofeli wachukue digrii, sijui wanasiasa hawa nao walifeli! Profesa Kitila Mkumbo wa ACT aliandika andiko liliainisha ukomo wa wanafunzi UDOM wasiozidi 1,800 hatukumsikiliza, wakapelekwa 7,000.
“Profesa Idris Kikula nilipozungumza naye alisema kalazimishwa, angefanyaje, afukuzwe chuo? Walianza mgomo nikafuatilia kujua kuna nini, nilisema hawa watu lazima waondoke.
“Nilikuwa nasubiri Chuo cha Dodoma wote wagome, wangeondoka, wanasiasa wanalalamika, tuache siasa katika masuala ya msingi,” alisema Rais Magufuli.
Alisema baadhi ya watoto waliofukuzwa ni wa viongozi, waliopelekwa huku wakiwa wamefeli na kwamba fedha ambazo zingetumika kuwalipia waliofaulu zinakwenda kuwalipia waliofeli – vilaza.
“Waliofaulu daraja la kwanza na la pili tutawatafutia njia nyingine ya kusoma, waliofeli wakatafute vyuo vya ‘saizi’ yao, haiwezekani huku wafanyakazi hewa, ukienda huku wanafunzi hewa.
“Mzee wangu umeniachia kazi ngumu kweli, badala ya fedha ziende kulipia madawati na kujenga maabara, zinakwenda kulipia vilaza,” alisema.
MIKOPO VYUO VIKUU
Aidha Rais Magufuli aliahidi kuwa Serikali yake itahakikisha inatoa mahitaji ya wanafunzi ikiwemo mikopo na kuboresha miundombinu ya vyuo, lakini akawataka wanavyuo nao kuwa wavumilivu na wazalendo pale ambapo mahitaji hayo yatachelewa kutokana na mchakato wa kuyapata kuhitaji muda.
Alisema Serikali yake ya awamu ya tano itahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo, lakini hatakubali kuielekeza kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
“Tumedhamiria kutoa elimu bora kwa Watanzania na tumejipanga kuhakikisha tunakabiliana na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyuo,” alisema.
Lakini Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi waliodahiliwa na baadhi ya vyuo hapa nchini pasipo kuwa na sifa zinazowawezesha kujiunga na chuo kikuu.
“Wapo wanaokopeshwa mikopo hii ya elimu ya juu lakini hawana sifa, mheshimiwa Profesa Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) nakushukuru kwa hatua unazozichukua katika kusafisha wizara yako na hili nalisema kwa uwazi, na ukweli lazima usemwe hata kama ni mbele ya wanachuo.
“Una D, D unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa Serikali, ni aibu ya ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani. Lakini wakati tunawalipia wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D, D manaake wengine ni divisheni 4, kuchukua digrii, wapo wanafunzi wengine wa kidato cha sita wamekosa mikopo, wapo wanafunzi wengine walio na diploma wamekosa mikopo,” alisema Rais Magufuli.
OMBI KWA WANACHUO
Rais Magufuli pia amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini kuacha kujihusisha na masuala ya siasa na badala yake wazingatie jukumu lililowapeleka vyuoni ambalo ni kusoma, huku akibainisha kuwa Serikali yake haitavumilia vitendo vya vurugu vyuoni.
“Ifike mahali Watanzania tukubali ukweli, tuache siasa kwenye masuala ya msingi, ukimpeleka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye ufaulu wa divisheni 4, anachukua digrii, akishatoka pale, hata kama atafanikiwa kupata digrii itakuwa ni ajabu.
“Lakini niwaombe wanafunzi mahali kote, msitumiwe na wanasiasa, mmekuja kusoma, someni, siasa mtazikuta mkiondoka, nawaambia mmekuja kusoma someni, na ndiyo maana hata katika kutoa mikopo hatubagui, sijui huyu CCM, sijui huyu Chadema, sijui huyu nini, nyie wote ni Watanzania, ndio lengo letu,” alisema.
KIKWETE
Rais Magufuli kabla ya kuzungumza hayo, alimpa nafasi ya kuzungumza Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Kikwete.
Kikwete alisema tangu alipokabidhiwa majukumu hayo alikutana na viongozi mbalimbali na kubaini changamoto zinazokikabili chuo hicho.
“Chuo kina mahitaji makubwa ya miundombinu, yakiwamo mabweni, asilimia 30 ya wanafunzi ndio wanaokaa chuoni, asilimia 70 wanaishi nje, mazingira wanayoishi si rafiki.
“Unaweza kuisoma vizuri barua yangu niliyokuletea jana, kuna hesabu nyingi tumeweka, kuna mahali tunahitaji bilioni 42, kwingine 30, ile kazi uliyonipa ukitaka yafanikiwe, haya yaliyomo katika barua yangu yafanyike.
“Suala la mikopo, wengi wangependa wapate, ipatikane kwa wakati, sasa mzee ukitaka nifanye ile kazi kwa ufanisi nisaidie yaleee, nitafanya kwa ufanisi, barua yangu nimeeleza mengi, hali ni nzuri, tunahitaji kuboresha,” alisema.
MAJIBU YA JPM
Akimjibu Kikwete, Rais Magufuli alisema: “Sikutarajia kama siku moja ungekuja kuniomba mimi hela, wakati mimi ndio nilikuwa naomba kwako hela.
“Nakushukuru kwa dhati si kwa unafiki, umetafuta dola za Marekani zaidi ya milioni 41 kwa ajili ya ujenzi wa maktaba, sikushiriki kutafuta hizo fedha, wewe ndio ulizitafuta, mimi nakuja kuweka jiwe la msingi tu.
“Naishukuru China, ni rafiki wa kweli asiye na masharti, masharti yanaudhi, fedha walizotoa wangetoa wengine masimango, bora tusisimangwe wakae na hivyo wanavyotaka kutupa,”alisema.
Akizungumzia maombi ya Kikwete, Rais Magufuli alisema akiamua kutoa fedha mahali akazipeleka UDSM atakuwa hajafanya kosa.
“Nitatoa kwa masharti, eneo la chuo kubwa, Mlimani City nimeambiwa inaingiza Sh bilioni 1.3 kwa mwaka, fedha za mwaka huu zitatumika vizuri, litengwe eneo yajengwe mabweni, tunaweza tusimalize kwa mwaka mmoja lakini tutakuwa tumeanza.
“Nitatafuta Sh bilioni 10, fedha za awali anazolipwa mkandarasi ni asilimia 50, hizo Sh bilioni 10 bado haziwezi kumalizika kwa malipo hayo, tafuteni eneo, nikivamia nione kazi, tangazeni tenda, tafuteni kandarasi hata akianza kesho kazi, nawahakikishia sitakosa kiasi hiki cha kuanzia,” alisema.
Rais Magufuli aliyaomba mashirika ya hifadhi ya jamii ya PPF na NSSF kujenga majengo na kuwapangisha wanafunzi katika maeneo ya chuo, badala ya kujenga pembezoni ambako hakuna wapangaji.
PONGEZI
Rais Magufuli pia alimpongeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Yunus Mgaya na kusema watu walitaka kumuingizia maneno ya hovyo akasimama hadharani, hataki vihiyo.
“Umetolewa uenyekiti TCU, nitakupa uenyekiti mwingine, mimi si ndiyo Rais, umeonyesha uzalendo wa kuwajibu wale,” alisema.
DARTS
Rais Magufuli amewashangaa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwanyamazia watu wanaoharibu miundombinu ya mradi wa mabasi ya mwendo kasi, ikiwamo kulala katika vituo na kujisaidia.
“Tumeleta mradi wa mabasi ya mwendo kasi, watu wanajisaidia humo, mkuu wa mkoa, wilaya, polisi wapo. Wapelekeni wakajisaidie gerezani.
“Trafiki wakamate magari yanayopita katika njia ya magari ya mwendo kasi wayapeleke vituoni, alafu watoe matairi… mwenyewe akija akiuliza mjibuni yalikuja hivyo hivyo,” alisema Rais Magufuli.
BALOZI WA CHINA
Naye Balozi wa China hapa nchini, Lu Youqing akizungumzia maktaba hiyo yenye ukubwa na ya kisasa miongoni mwa maktaba zote zilizojengwa na Serikali ya China barani Afrika, alisema ujenzi wake utagharimu dola za Marekani milioni 40.
“Matumaini yangu kukamilika kwa maktaba hii inaweza kuboresha mazingira ya ufundishaji UDSM, itakuwa jukwaa muhimu kwa kufundisha wanafunzi na itasaidia mawasiliano ya utamaduni baina ya nchi zetu mbili.
“Ninatumaini Kampuni ya Ujenzi ya Jiangsujiangdu inaweza kushirikiana vizuri na mamlaka husika ya chuo kukamilisha kazi ya ujenzi,” alisema.
Maktaba hiyo ya kisasa inayojengwa itakapokamilika itakuwa ndiyo bora kuliko zote barani Afrika, ikiwa na ukubwa wa eneo la meta za mraba 20,000 na uwezo wa kuwa na vitabu 800,000 na kuchukua wanafunzi 2,600 kwa mpigo.
Post a Comment